Jumapili 25 Oktoba 2026 - 13:25
Kongamano la Kumuenzi Shahidi Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini na Kuchunguza Mwenendo Wake wa Kielimu na Kivitendo Lafanyika Najaf Ashraf

Hawza/ Kongamano la kumuenzi na kuchunguza mwenendo wa kielimu na kivitendo wa Shahidi Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini (Quddisa Sirruh), lilifanyika Alhamisi, tarehe 30 Mehr 1405 Hijria ya Shamsia, sawa na tarehe 22 Oktoba 2026, katika Husainiya ya Imam Ridha (a.s.) mjini Najaf Ashraf, likihudhuriwa na maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu kutoka Iran, Iraq na nchi nyingine.

Kwa mujibu wa Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza, kongamano hilo la kumuenzi na kuchunguza mwenendo wa kielimu na kivitendo wa Shahidi Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini (Quddisa Sirruh) liliandaliwa na ofisi ya uwakilishi wa Taasisi ya Kusimamia na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini (r.a.) nchini Iraq. Kongamano hilo lilifanyika Alhamisi, tarehe 30 Mehr 1405 Hijria ya Shamsia, sawa na tarehe 10 Jamad al-Ula, saa 3:30 asubuhi, katika Husainiya ya Imam Ridha (a.s.) iliyopo katika mji wa Najaf Ashraf.

Shughuli za kongamano hilo zilianza kwa kusomwa aya za Qur'ani Tukufu na Haj Karim Mansuri. Baada ya hapo, Hujjatul-Islam Ramadhani, mkurugenzi wa tawi la Najaf la Taasisi ya Kusimamia na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini, aliwakaribisha maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu waliohudhuria, kisha akatangaza kuanza rasmi programu hiyo.

Baadaye, Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Komsari, rais wa Taasisi ya Kusimamia na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini, alikuwa mzungumzaji wa kwanza katika kongamano hilo. Katika hotuba yake, alielezea juhudi za kujitolea na shughuli za mapambano zilizofanywa na Shahidi Sayyid Mustafa Khomeini, pamoja na nafasi yake ya kipekee katika harakati za mapambano na kuambatana na Imam Khomeini (Quddisa Sirruh).

Kisha, Ayatullah Sayyid Mojtaba Husaini, mwakilishi wa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iraq, alieleza vipengele mbalimbali vya mwenendo wa kielimu na kivitendo wa Shahidi Sayyid Mustafa Khomeini. Akigusia sifa zake za kibinafsi na kielimu, alifafanua nafasi yake mashuhuri katika nyanja za elimu na utekelezaji wa vitendo.

Katika sehemu iliyofuata, Ayatullah Sayyid Fadhil al-Jabiri, miongoni mwa walimu wa masomo ya juu ya ijtihadi (Dars Kharij) katika Hawza ya Najaf, alichunguza kazi za tafsiri ya Qur'ani zilizoandikwa na Shahidi Sayyid Mustafa Khomeini. Akisisitiza mkabala wake wa kielimu na fikra zake za kina katika kufasiri Qur'ani Tukufu, alieleza na kufafanua umuhimu wa urithi wake katika taaluma ya tafsiri ya Qur'ani.

Vilevile, Profesa Muhammad Rabii, mmoja wa walimu mashuhuri wa ngazi za juu za masomo katika Hawza ya Najaf, katika hotuba yake alizungumzia nafasi ya kielimu ya shahidi huyo na jukumu la maulamaa na wanafikra wa Kiislamu katika jihadi ya kielimu na kutetea maarifa na mafundisho ya Uislamu. Pia alisisitiza umuhimu wa juhudi za kielimu za maulamaa katika kulinda tunu na mafundisho ya Kiislamu.

Kwa ujumla, kongamano hilo lilitoa fursa ya kuchunguza vipengele mbalimbali vya utu wa kielimu, kivitendo na kijihadi wa Shahidi Sayyid Mustafa Khomeini. Aidha, kwa kujadili mwenendo wake wa kielimu na kivitendo, kazi zake za tafsiri ya Qur'ani na nafasi yake katika elimu, kongamano hilo lilisisitiza umuhimu wa kuufahamu na kuutambulisha urithi wa fikra na elimu wa shahidi huyo mkubwa, pamoja na kuendeleza tafiti kuhusu kazi na mawazo yake.

Inafaa kutajwa kuwa katika sehemu ya mwisho ya hafla hiyo, kitabu kilichoitwa “Maisha na Mapambano ya Ayatullah Sayyid Mustafa Khomeini” kilizinduliwa rasmi.

Programu hiyo iliandaliwa katika juhudi za kuhifadhi urithi wa kielimu na kivitendo wa Shahidi Sayyid Mustafa Khomeini na kutambulisha vipengele mashuhuri vya utu wake kwa watafiti, wanafunzi wa Hawza na wanazuoni wa Hawza ya Najaf Ashraf.

Inapaswa pia kufahamika kuwa washiriki wa hafla hiyo walitoka katika mataifa mbalimbali, yakiwemo Iran, Iraq, Bangladesh, Morocco na mataifa mengine.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha